Mitandao ya kijamii, intaneti kichocheo uzazi wa ‘kisu’

UKUAJI wa sayansi na teknolojia unatajwa kuwa sababu kubwa ya ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji hapa nchini. Mahojiano yaliyofanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka vituo tofauti vya afya na hospitali wanabainisha hilo. Wataalamu hao wamesema mitandao ya kijamii imekuwa na ushawishi mkubwa zaidi kwa wanawake kufanya maamuzi wakati wa kujifungua. Lakini si hilo tu mtindo mbaya wa maisha, ulaji na kutokufanya mazoezi kunakochangiwa na ukuaji wa teknolojia nako kunachangia. Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inaonesha kuwa kujifungua kwa upasuaji sasa imekuwa suala la kawaida ikiainisha kuwa kati ya wanawake watano mmoja hujifungua kwa upasuaji sawa na asilimia 21 ya uzazi wote. Ni tofauti na awali ambapo mwaka 1990 asilimia saba tu ndio waliopatiwa huduma ya upasuaji kutokana na dharura ya kushindwa kujifungua kawaida. WHO imeonya ongezeko zaidi la hadi asilimia 29 katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Inasema ifikapo mwaka 2030 viwango vya juu vinaweza kuwa Asia ya Mashariki ikitarajiwa kufika asilimia 63, Amerika ya Kusini na Caribbea asilimia 54, Asia ya Magharibi asilimia 50, Afrika ya Kaskazini asilimia 48, Kusini mwa Ulaya asilimia 47, Australia na New Zealand asilimia 45. Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Palestina, Dar es Salaam, Idrissa Kabanda, anasema wanawake wanaomba kufanyiwa upasuaji hata kama hawana changamoto za kiafya. “Kwasababu amepata taarifa kwenye mitandao ya kijamii au amesikia mtaani anakuja na mawazo ambayo ameshapanga. Akija hapa anaomba kujifungua kwa operesheni.” Dk Kabanda anasema sababu nyingine ni mabadiliko ya mfumo wa maisha ikiwemo ulaji na kutofanya mazoezi. “Kuna tatizo la ongezeko la uzito mkubwa kwa wanawake na pia vyakula wanavyokula vina madhara ya baadae kama magonjwa sugu yanaweza kuwa sababu ya kujifungua kwa operesheni. Anasema ulaji pia hufanya mtoto kuwa na uzito mkubwa. Anasema takwimu za Hospitali ya Palestina zinaonesha kuwa wastani wa wanawake 150 hadi 170 hujifungua kwa njia ya upasuaji huku wanaojifungua kwa kawaida ni 500 hadi 700 kwa mwezi. Dk Living Colman ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema ingawa ni haki ya mgonjwa kuchagua huduma, wanawake sasa wanafuatilia namna ya kujifungua kupitia mitandao ya kijamii hali inayowatia wasiwasi wa uchungu wakati wa kujifungua. “Matumizi ya mitandao kama magroup ya whatsapp, youtube ambavyo mama anaona jinsi mtu anavyojifungua hivyo huingia woga na kuamua kuchagua njia ambayo anaona ni rahisi. “Lakini suala la upasuaji wakati wa uzazi linatakiwa kuwa na sababu na pale mgonjwa anapochagua bila sababu ataelezwa faida na hasara zake kama bado anasisitiza basi ni haki yake,” anabainisha. USHAWISHI WA MITANDAO  Kupitia uchunguzi uliofanywa kwa msaada wa Taasisi ya CHIMBUA, wanawake wanaoomba kufanyiwa upasuaji hawana uelewa kuhusu faida na madhara. Mmoja wa wanawake waliowahi kuomba kufanyiwa upasuaji, Nasra Baziri, anasema wasiwasi alioona kupitia mtandao wa youtube ulimfanya kutamani kujifungua kwa njia hiyo. “Ilinifanya kuwa na maamuzi ya kutaka kufanyiwa upasuaji, nilikutana na daktari ambaye alinieleza faida na hasara baada ya hapo nikafanya maamuzi ya kujifungua bila upasuaji. “Ule uchungu ulikuwa wa muda mfupi na mtoto amekua na anaendelea vizuri,” anasema Nasra. Si hilo tu wanawake wengine wanaeleza kuhofia kutanuka kwa maumbile yao. Mmoja wa wanawake hakutaka jina lake kuandikwa anasema alisikia kupitia mtandao kuwa endapo atafanyiwa upasuaji maumbile yake ya uke yatabaki kama awali. “Hilo ndilo lililonivutia zaidi kufanyiwa upasuaji,” anaeleza. MADHARA YA UPASUAJI WAKATI WA KUJIFUNGUA  Cosolata Kimathy ni mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam na mama wa watoto wanne. Ingawa hajafanyiwa upasuaji kwa uzazi wa mtoto wa kwanza na wa pili lakini mtoto wake wa tatu na wa nne alifanyiwa kutokana na hatari iliyokuwepo. “Mtoto wa tatu ni kwasababu alikuwa mkubwa hivyo madaktari wakaniambia ninatakiwa kufanyiwa upasuaji ilikuwa mwaka 2010. “Mtoto wa mwisho nilifanyiwa upasuaji japo sikutamani kutokana na matatizo ilinilazimu,” anasema. Sasa ni miaka12 tangu amefanyiwa upasuaji anasema bado madhara ya upasuaji yanamtatiza. “Shida kubwa ninayopata ni maumivu katika mshono wakati wa baridi kutokana na hali hii nashindwa kufanya kazi wakati mwingine ni mateso,” anasimulia. Mwanamke mwingine, Rose Mwita, mama wa watoto watatu anasema baada ya kujifungua kwa upasuaji miaka saba iliyopita sasa anakumbwa na maumivu ya mgongo. MADAKTARI WAELEZA Mtaalamu wa afya ya uzazi na elimu kwa vijana kutoka Hospitali ya Marie Stopes Mwenge, Dk Mashingo Lerise, anasema si mara zote madhara hujitokeza baada ya upasuaji yanaweza kuchukua muda mrefu. Anaeleza kuwa kawaida mama anashauriwa kufanyiwa upasuaji kwa wastani mara tatu, si kwamba inakatazwa zaidi lakini inakuwa hatari kwake. “Sababu za kufanyiwa upasuaji ni magonjwa sugu kama presha, maumbile ya nyonga ya mama kushindwa kutanuka. Anasema kuna upasuaji wa dharura kama vile mama kuwa na uchungu na njia kutofunguka mtoto inabidi atolewe kwa haraka na mapigo ya moyo ya mtoto kupungua au kwenda haraka. “Mtoto kujisaidia tumboni na mama kutoka damu nyingi. Katika hili, Dk Kabanda anasema madhara ya muda mfupi ni gharama za kuuguza kidonda na maumivu badala ya kumuhudumia mtoto. Anasema wakati wa baridi mshono unapata maumivu na pia dawa za sindano ya ganzi ambazo wanachomwa mgongoni zinaweza kuwaathiri. “Inawezekana wakati wa operesheni njia walizotumia kumchoma mama hazikuwa nzuri, wakati wa kumchoma mama alikuwa hajatulia,” anasema. Anasema hakuna uhusiano wa maumbile ya uke kutanuka na kubaki hivyo kwa kuwa amejifungua kwa njia ya kawaida bali ni upotoshaji ambao unapaswa kukemewa na kupuuzwa. Wataalamu mbalimbali wa afya ya uzazi wanaeleza kuwa, sehemu ya uke wa mwanamke ni kama mpira hivyo hutanuka wakati mtoto anapita na kurejea kawaida baada ya kipindi kifupi cha uzazi. Dk Kabanda anasema wanawashauri kutofuata taarifa za kwenye mitandao kwani nyingi si sahihi hivyo wapate taarifa kutoka kwa wataalamu. WANAUME WANENA Saimon Furahini, mkazi wa Dar es Salaam anasema kuwa si jambo jema kwa wanawake kutaka kujifungua kwa upasuaji ikiwa hakuna haja. “Waache kuiga maisha na kuharibu asili ya uumbaji kama anaweza kujifungua kawaida afanye hivyo na kuna wanaume ambao wanawashawishi wake zao kufanyiwa upasuaji bila sababu. MAZOEZI YA MAMA ALIYEFANYIWA UPASUAJI Mtaalamu wa mazoezi tiba MNH anasema madhara yatakayompata mama asipofanya mazoezi ni kupata mkazo wa misuli ya mwili, kukosa nguvu na kupoteza ubora. “Atafundishwa namna anaweza kupumua, jinsi ya kukohoa bila kuathiri sehemu anapofanyiwa upasuaji, mkao sahihi wakati wa kunyonyesha na kugeuka kitandani,” anasema. Anasema baada ya siku saba atafundishwa kufanya mazoezi ya tumbo na nyuzi zinatolewa kama hakuna tatizo zaidi. JE, SERA YA AFYA INASEMAJE? Tamko la sera inasema serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha afya ya uzazi ya wanawake na wanaume, watu wenye ulemavu, vijana na wazee. Na pia inaeleza kuwa serikali itaandaa miongozo, mikakati na kuratibu shughuli zinazolenga afya ya uzazi ya makundi mbalimbali pamoja na kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinatekelezwa. Inasema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha utoaji wa huduma bora za uzazi katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazowavutia wanawake, wanaume na vijana. Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kuna haja ya kuwa na sera inayoelekea moja kwa moja kwenye suala la upasuaji wakati wa kujifungua. MAPENDEKEZO YA WHO  WHO inapendekeza hatua zingine zisizo za kitabibu ambazo zinaweza kupunguza uzazi wa njia ya upasuaji usio wa lazima. Njia ambazo zinapendekezwa ni utoaji wa elimu kwa wanawake kupanga namna bora ya kujifungua ikiwemo warsha za maandalizi ya kujifungua, programu za kupumzika na msaada wa kisaikolojia kwa wenye hofu ya maumivu.

Add a Comment

Your email address will not be published.

All Categories

Get Free Consultations

SPECIAL ADVISORS
Quis autem vel eum iure repreh ende