Mwitikio wa wasichana kusoma ufundi waongezeka

Na Mwandishi Wetu, Dodoma Imeelezwa kuwa kwasasa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wasichana kujiunga na fani za ufundi tofauti na awali ambapo fani hiyo ilidhaniwa kuwa ni ya wanaume pekee. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Ajira,  Vijana na Watu wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako, ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Vyuo vya ufundi vya Don Bosco na VETA ambao wananufaika na mipango ya kukuza ujuzi kitaifa inayotekelezwa na ofisi hiyo. Amesema fani zinazotolewa kwenye mpango huo ni ufundi wa magari, useremala, uashi, upishi, huduma za vyakula na vinywaji, ufundi umeme, uchomeleaji vyuma, ufundi bomba, uchongaji vipuri na ushonaji wa nguo. Amesema awali mwamko wa watoto wa kike kujiunga ulikuwa mdogo wakiwa na dhana potofu kuwa ufundi ni kwa ajili ya wanaume tu. Prof.Ndalichako amesema utekelezaji wa mpango huo unalenga kukabiliana na tatizo la ujuzi na kuendelea kutoa wito kwa wazazi kuwaruhusu watoto wao wa kike kujiunga na fani hizo. Aidha, amesema kupitia programu hiyo ya mafunzo ya uanagenzi na uzoefu kazini kwa mwaka wa fedha 2021/22, vijana 22,200 wamepata mafunzo. Awali, Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Don Bosco, Padri Boniphace Mchami, amesema wakati walipoanza kutekeleza program hiyo kulikuwa na changamoto ya mila na desturi potofu juu ya mtoto wa kike kuwa na uhuru wa kujiunga na fani yoyote jambo ambalo wanaendelea kulitatua ili kupata wanafunzi wengi zaidi wa kike kwenye fani hizo. Mmoja wa vijana wanaonufaika na program hiyo katika chuo cha VETA, Neema Mushi, ameshukuru serikali kwa kutoa mafunzo ya fani hizo kwa vijana ambao wengi walikuwa majumbani na hawakuwa na shughuli za kuwaingizia kipato.

Add a Comment

Your email address will not be published.

All Categories

Get Free Consultations

SPECIAL ADVISORS
Quis autem vel eum iure repreh ende