Rais Samia aendelea kuzoa tuzo
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Rais Samia Suluhu Hassan ametangazwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Watetezi na Amani kuwa mshindi wa tuzo mbili za kimataifa ikiwemo ya amani duniani 2022, ikiwa ni miezi mitatu baada ya kupokea tuzo nyingine ya Babacar Ndiaye Trophy 2022.
Tuzo nyingine aliyotangazwa kuwa mshindi akiwa ni Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuipata ni tuzo ya Rais wa Dhahabu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Gaudentia Kabaka amesema Rais Samia alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hizo wiki iliyopita na atakabidhiwa tuzo hizo Oktoba 24, mwaka huu.
Amesema miongoni mwa mambo yaliyomfanya Rais Samia kupata tuzo hizo ni uboreshaji wa miundombinu ya afya na elimu ndani ya kipindi kifupi, utetezi wa masuala ya amani ikiwemo uhuru wa kuabudu na amani na kujali masuala ya kijinsia kwa kuteua wanawake wengi katika uongozi.
“Sisi UWT na wanawake wote wa Tanzania tumeona fahari sana kwa kuwa na Rais mwanamke ambaye ni Mheshimiwa Samia. Rais wa kwanza Afrika mwanamke kushinda tuzo mbili na kuandika historia ya kipekee nchini,”anasema.
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Maendeleo, (Wajiki) Janeth Mawinza amempongeza Rais Samia kwa kupata tuzo.
“Tuzo hizo ziwe kichocheo kwake katika kuimarisha masuala mbalimbali yaikiwemo ya kijinsia,”anasema.
Amemuomba Rais Samia kuangalia masuala ya ukatili wa kijinsia hasa katika ulinzi na usalama wa watoto ambacho kimekuwa ni kilio kikubwa hivi sasa nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie amesema Rais Samia anastahili kupata tuzo hizo kwasababu ni mtu wa kuchangamana na dunia na ameweza kujijengea taswira nzuri katika medani ya kimataifa.
Ameongeza kuwa kuna mabadiliko makubwa katika masuala ya demokrasia na siasa ikiwemo kuongezeka kwa uhuru wa kutoa maoni, kukosoa na kujumuika ingawa hata kama bado haijafunguliwa sana.
“Amejaribu kufanya maridhiano na vyama vya siasa, amekutana na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe) mara kadhaa, amemlipa Lissu mafao yake…Hata katika suala la Katiba ameunda kamati na watu wametoa maoni yao. Nchi imetulia,”amesema.
Maraisi waliowahi kupata tuzo hizo kwa bara la Afrika ni Rais wa Liberia George Ulah na Rais wa Botswana Seretse Ian Khamu.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kupokea tuzo ambapo Mei 22,2022 alipokea tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 (Babacar Ndiaye Trophy 2022) ikiwa ni kutambua jitihada zake katika ujenzi wa miundombinu.
Recent Posts
admin0 Comments
Heavy rains raises concerns
Joyce Bazira0 Comments
Siku ya Wazee Dunia; Tanzania ina mengi ya kujivunia?
Joyce Bazira0 Comments