Mabadiliko ya tabianchi mzigo mkubwa kwa wanawake

WAKATI wana harakati na viongozi wa ngazi mbalimbali kitaifa na kimataifa wanaendelea kutatuta mbinu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, imebainika kuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko hayo ni wanawake na watoto wa kike.

Adeline Joseph, Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Mama Kwanza, anasema mabadiliko hayo yanachukuliwa kama aina mpya ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kwani athari zake huyafanya makundi hayo yanyanyasike zaidi.

Mario Masanja, Mwenyekiti wa Mazingira ni Uhai, taasisi inayojishughulisha na utunzaji wa mazingira, anasema maeneo yanayoathiriwa zaidi na mabadiliko hayo, huwagusa moja kwa moja wanawake na wasichana

Kwa mujibu wa Bw. Masanja, mabadiliko ya tabianchi husababisha ukame kuongezeka, hali ambayo inaathiri upatikanaji wa chakula kwa binadamu na wanyama; kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo yanayotegemea mvua kwa asilimia kubwa; kuongezeka kwa matukio ya mafuriko makubwa ambayo huharibu mali,miundo mbinu na kusababisha vifo vya watu na wanyama.

Anataja matokeo mengine ya mabadiliko hayo kuwa ni kuwepo kwa vipindi virefu vya joto kali na ukame, vinavyosababisha kupungua kwa upatikanaji wa maji, mvua zisizotabirika, mafuriko, kuongezeka kwa joto kali, vimbunga na vingine vingi.

Maria George, Katibu wa taasisi ya Mama Kwanza anasema mabadiliko ya tabianchi huathiri shughuli nyingi zikiwemo za kilimo, ufugaji, uvuvi na nyinginezo, hali inayosababisha rasilimali muhimu katika familia kupungua na kumuongezea mzigo mwanamke.

“Kukiwa na shida ya maji anayehangaika ni mama, kukiwa na kiangazi cha muda mrefu, baba atahamisha mifugo na mwanawe wa kiume akimuacha mama na watoto wa kike wakihangaika’’ anafanua Bi. Maria

Simon Kileo, Katibu wa taasisi ya Mazingira ni Uhai anasema ingawa wanaume wana maamuzi kuhusu umiliki na matumizi ya rasilimali za kijamii na kiuchumi, lakini wazalishaji wakubwa hasa kwenye kilimo ni wanawake, na kwamba kilimo kinapoathirika,familia nzima hutetereka.

``Kwa kuwa wahusika wakuu katika shughuli nyingi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi ni wanawake, mabadiliko hayo huwagusa moja kwa moja,’’ anasema Bw. Kileo

Kwa mujibu wa Bw. Kileo, majukumu yao kama walezi na wanaohudumia familia kwa karibu zaidi huwafanya wanawake kuwa katika mazingira hatari zaidi wakati wa majanga yanayosabishwa na mabadiliko ya tabianchi kama mafuriko na ukame.

Aidha Bw. Kileo anafafanua kuwa kutokana na mabadiliko hayo, wanawake wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta kuni na maji, huku wanaume wengi wakihama kutafuta malisho au kazi na kuziacha familia chini ya mama, ambaye kipato chake kinakuwa tayari kimeshuka kutokana na mabadiliko hayo.

Kwa mujibu wa Bw. Kileo, mabadiliko ya tabianchi, huathiri pia afya ya wanawake.

``Unapotokea ukame, chakula kinachopatikana ni kidogo, lakini mama atahakikisha watu wote wa nyumbani kwake wamekula hata kama yeye atabaki na njaa, hilo litamfanya ataathirike kiafya,’’ anasema Bw. Kileo.

Nini kifanyike kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

``Hatua ya kwanza ya kutafuta ufumbuzi wa mabadiliko ya tabianchi ni kila mwananchi kuepuka shughuli zinazochochea mabadiliko hayo ,’’anasema Mwenyekiti wa taasisi ya Mazingira ni Uhai, Bw. Mario Masanja.

Kwa mujibu wa Bw. Masanja kwa kiasi kikubwa shughuli za mwanadamu zisizozingatia utunzaji wa mazingira zimekuwa zikichangia uwepo wa mabadiliko ya tabianchi.

``Kwa mfano uandaaji wa mashamba makubwa unaohusisha uchomaji moto, shughuli za viwanda, ukataji miti, uchomaji wa mkaa na shughuli nyingine zinazofanywa na watu katika harakati za kutafuta riziki ni miongoni mwa vitu tunavyotakiwa kuepuka ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,’’ anafafanua.

Anasema kwa watu wa kawaida wanaweza kuona mabadiliko hayo kama hayawahusu lakini wakielimishwa namna wanadamu wanavyochangia kuwepo kwa hali hiyo na jinsi athari zake zinavyoathiri watu, wataelewa na kuanza kuchukua hatua.

Akizungumzia nini kifanyike, Adeline Joseph, Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Mama Kwanza ansema, jitihada mahsusi na za haraka zinahitajika kuchukuliwa ili kupunguza visababishi vya mabadiliko ya tabianchi.

``Tuongeze kasi na idadi ya upandaji miti, tuache matumizi ya kuni na nishati ambayo inapelekea kuharibu misitu, badala yake tutumie nishati mbadala kama gesi, bayogesi, umeme na umeme wa jua,’’ anashauri Bi. Adeline.

Na Joyce Bazira

Add a Comment

Your email address will not be published.

All Categories

Get Free Consultations

SPECIAL ADVISORS
Quis autem vel eum iure repreh ende