Siku ya Wazee Dunia; Tanzania ina mengi ya kujivunia?
Ni Jumamosi asubuhi. Kwa mbali jua limeanza kuchomoza na kutengeneza nuru inayoipamba siku hii mpya. Katikati ya shamba la migomba, kuna nyumba kubwa ya udongo yenye bati kuu kuu. Hatua chache kutoka kwenye nyumba, kuna mti wa kivuli ambao, chini yake kuna gogo kubwa. Kama afanyavyo siku zote asubuhi, Mzee Jackson Malebo, leo ameketi kwenye gogo lakini tofauti na siku nyingine, leo amevalia nadhifu na uso wake umechangamka. Majirani wanamshangaa, wanajiuliza maswali bila majibu, kila mtu anawaza lake. Kitu gani kipya kimetokea katika maisha ya Mzee Malebo? Fuatana na Mwandishi wa Makala haya Joyce Bazira kujua zaidi.
Wakati Oktoba Mosi kila mwaka, mataifa yote duniani huadhimisha Siku ya Wazee Duniani, Tanzania inasherehekea siku hiyo ikiwa na mengi ya kujivunia kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kushughulikia kero za wazee.
Mzee Malebo ni kielelezo cha wazee wengine nchini kote, ambao maisha yao yamebadilika. Kutokana na mikakati iliyowekwa na wadau wakishirikiana na Serikali, wazee nchini hivi sasa wamepata matumaini mapya na wana matarajio ya kuishi bila hofu huku wakipata stahiki zao bila usumbufu
Mabaraza ya wazee yameleta matumaini mapya kwa wazee
Kuanzishwa kwa mabaraza ya wazee katika mikoa karibu yote Tanzania Bara ni miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanyika kuhakikisha kunakuwa na mfumo mzuri wa kuwafikia wazee kwa haraka na kushughulikia changamoto zao kwa ufanisi.
Mabaraza hayo yako katika ngazi mbalimbali kuanzia kijiji, kata, wilaya na mkoa na mpango wa kuanzisha baraza moja la taifa lenye uwakilishi wa wazee kutoka kila mkoa uko mbioni.
`` Wazee sasa wana majukwaa ya kuzungumza masuala yao kwa uhuru na bila hofu. Kupitia mabaraza hayo pia wanapata taarifa muhimu zinazowahusu na migogoro mingi inayowahusisha wazee inapatiwa ufumbuzi kwa haraka na bila usumbufu wowote,’’ anasema Mkurugenzi wa Shirika la Kuhudumia Wazee Tanzania, HelpAge International, Bw. Daniel Smart katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya.
Kwa mujibu wa Bw. Smart, hadi sasa mabaraza yanafanya kazi nzuri ya kupokea na kuyatafutia ufumbuzi masuala mbalimbali yanayowahusu wazee. ``Changamoto nyingi zinazowakabili wazee zinamalizwa katika mabaraza huko huko maeneo wanayoishi, zile zenye sura ya kitaifa ndizo hufikishwa ngazi ya juu kupatiwa ufumbuzi,’’ anafafanua Bw. Smart
Juni 15 mwaka huu, wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi Wazee yanayoadhimishwa kila mwaka, Waziri wa Afya na Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Gwajima alisema kuwa Serikali inatambua kuwa wazee ni hazina ya taifa kutokana na ujuzi na uzoefu walio nao katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na katika kuhakikisha kuwa hazina hii inatumika ipasavyo, Serikali imeendelea na uundaji wa mabaraza ya wazee kote nchini.
Alisema jumla ya mabaraza 14,883 yameundwa kuanzia ngazi ya Vijiji/Mitaa, Kata, Wilaya na mikoa nchini.
Bw. Joseph Mbasha, Meneja Miradi anayeshughulikia Ulinzi wa mahusiano ya kitaasisi kutoka shirika la HelpAge International, anataja mafanikio mbalimbali yanayotokana na mabaraza hayo tangu kuanzishwa kwake.
``Huko Kahama, kupitia baraza la wazee, watu walihamasishwa kuwakatia bima za afya wazee 300; mkoani Simiyu, baraza la wazee lilifanikiwa kuzuia matukio ya mauaji ya wazee yanachochewa na imani za kishirikina na huko Karagwe, mabaraza yamefanikiwa kuwaelimisha watu juu ya dhana nzima ya uzee na sasa wana uelewa mpana na wanawajibika katika kuwahudumia’’ anasema.
Kwa mujibu wa Bw. Mbasha, mabaraza ya wazee pia yanasadia kuimarisha amani na mshikamano miongoni mwa wana jamii na kwa upande mwingine yanachochea uwajibikaji wa jamii na wananchi mmoja mmoja katika kuwajali na kuwahudumia wazee katika maeneo yao.
Anasema muundo wa mabaraza hayo ni mfano mzuri wa kuigwa na jamii nzima kwani unazingatia usawa wa kijinsia. Kila baraza lina wazee saba, wanaume kwa wanawake.
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mabaraza hayo, Mkurugenzi wa HelpAge International, Bw. Smart anasema bado mabaraza yanaendeshwa chini ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003, kwa kuwa hayajatungiwa sheria.
``Licha ya uwepo wa Sera ya Wazee na mipango mizuri ya Serikali, hali ya kutokuwa na sheria ya wazee kunasababisha mambo mengi kukosa msukumo wa kisheria na hivyo huduma kwa wazee kutolewa kwa hisani na huruma za kiongozi aliyepo,’’ anasema.
Hamasa kuhusu siku ya wazee dunia
Mafanikio mengine ambayo HelpAge na wadau wengine wanayojivunia wanapoadhimisha siku ya wazee duniani mwaka huu, ni kufanikiwa kuwajengea Watanzania uelewa juu ya umuhimu wa siku ya wazee duniani.
``Wakati tulipoanza kuadhimisha siku ya wazee, watu wengi hawakuwa na uelewa juu ya siku hii muhimu na kutokana na hilo, tulilazimika kuibeba peke yetu, lakini hivi sasa wadau wana uelewa wa kutosha na Serikali iko kwenye injini ikiratibu shughuli zitakazofanyika kwenye maadhimisho ya siku hiyo muhimu,’’anasema Bw. Smart.
Hivi sasa kila mdau wakiwemo wazee wenyewe wanaitambua Oktoba Mosi na kuithamini kama siku maalum kwao, anasema Bw. Smart na kuongeza kuwa ushirikiano mkubwa unaoonyeshwa na Serikali ni mafanikio makubwa ambayo hayatakiwi kuchukuliwa kiurahisi.
Akizungumzia maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya wazee duniani, Meneja Miradi anayeshughulikia Ulinzi wa mahusiano ya kitaasisi kutoka shirika la HelpAge International, Bw. Mbasha anasema, tofauti na miaka mingine, katika maadhimisho ya mwaka huu, wazeee hawatakutana eneo moja na badala yake watabaki kwenye mikoa yao ambapo kila mkoa utakuwa na shughuli zake na tayari Serikali imetoa mwongozo wa nini kifanyike, huku maafisa ustawi wa jamii wakipewa jukumu la kusimamia shughuli hizo katika mikoa yao
Kwa mujibu wa ratiba ya maadhimisho hayo, kuanzia Septemba 27 hadi Oktoba 1, kila mkoa ulitakiwa kuweka mabanda katika viwanja vya maadhimisho yanayoonyesha huduma mbalimbali kwa wazee. Miongoni mwa huduma hizo ni; huduma ya msaada wa kisaikolojia kwa wazee na familia zenye uhitaji; huduma za afya na chanjo ya UVIKO 19 na uelimishaji katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu maadhimisho na huduma kwa wazee.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, siku ya kilele cha maadhimisho, wazee kutoka halmashauri zote ndani ya mikoa, wananchi pamoja na wadau wengine washiriki kwa pamoja maadhimisho hayo.
Kwa mujibu wa Bw. Mbasha, kauli mbiu ya mwaka huu ni ``Matumizi Sahihi ya Kidijitali kwa Ustawi wa Rika Zote’’ ikimaanisha kuwa katika kipindi hiki cha UVIKO 19 ambako kuna taarifa nyingi za upotoshaji juu ya ugonjwa huo, ni vema kukawa na utaratibu wa kuhakikisha wazee wanasaidiwa kupata taarifa muhimu, sahihi na kwa wakati.
Kikao cha Waziri Gwajima, wadau kila wiki
Mafanikio mengine makubwa ni kuanzishwa kwa utaratibu mpya ambao unawawezesha wadau na Serikali kukutana mara moja kila wiki na kujadili changamoto zinazowakabili wazee.
Akifafanua kuhusu utaratibu huo, Dk. Edwin Mung’ong’o ambaye ni Meneja wa Afya na Huduma kutoka HelpAge International, anasema kikao hicho hufanyika kila Jumamosi na hushirikisha wizara mbili, yaani Wizara ya Afya na Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ile ya TAMISEMI idara inayoshughulikia masuala ya wazee, HelpAge International na wawakilishi wa wazee kupitia mtandao wa wazee Tanzania na Waziri wa Afya Dk. Dorothy Gwajima ndiye mwenyekiti wa kikao hicho.
``Huu ni utaratibu mzuri na wa kipekee. Uzuri wake ni kwamba wadau wote muhimu wanakuwa kwenye kikao kimoja na wakati changamoto zinazowakabili wazee zinazopowasilishwa, Waziri huwauliza wahusika mmoja mmoja ni kwa namna gani watazitafutia ufumbuzi kero hizo,’’ anasema Dk. Mung’ong’o, kabla ya kuongeza `` hali kama hiyo inamfanya mtu awajibike kufanyia kazi kero zilizoelekezwa eneo lake kwa sababu anajua asipofanya hivyo, siku ya kikao kinachofuata, lazima atabanwa’’
Kwa mujibu wa Dk. Mung’ong’o, upekee wa utaratibu huo unatokana na ukweli kuwa unatengeneza mfumo wa haraka wa uwajibikaji miongoni mwa watendaji wa Serikali na wadau wengine . Pia inakuwa rahisi kubaini kero sugu, yaani zile ambazo zimekuwa zikiwakabili wazee kwa muda mrefu sasa, na kuzitafutia ufumbuzi.
Kupungua kwa mauaji ya wazee
Mafanikio mengine ya kujivunia wakati wa maadhimisho ya mwaka huu ni kupungua kwa vitendo vya mauaji ya wazee kwa imani za ushirikina, mafanikio ambayo HelpAge wanasema yametokana na kampeni za wadau mbalimbali ikiwemo Serikali.
Juni 15 mwaka huu , katika hotuba ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaid Khamis alisema kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee nchini vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Alisema taarifa kutoka Jeshi la Polisi inaonyesha mauaji ya wazee yamepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 577 mwaka 2014 hadi wazee 34 Desemba 2020.
“Kutokana na ukweli kwamba hali duni ya kipato ni miongoni mwa sababu zinazochangia vitendo vya ukatili kwa wazee, serikali inalenga kuhakikisha wazee wanawezeshwa katika kubuni na kuendesha shughuli za ujasiriamali kupitia vikundi vidogo vidogo kwenye jamii, ili kuwawezesha kuinua kipato na kumudu mahitaji yao ya msingi,” alisema.
Hoja za msingi za wazee
Licha mafanikio yaliyofikiwa katika kupunguza changamoto zinazowakazili wazee nchini, Mkurugenzi wa HelpAge International, Bw. Daniel Smart anasema bado kuna maeneo kadhaa ambayo yanaleta kero kubwa kwa wazee nchini.
Andiko lenye changamoto za wazee lililowasilishwa kwa Waziri wa Afya Dkt. Gwajima katika kikao kazi kilichofanyika Septemba mwaka huu, kikihusisha wawakilishi wa wazee, Wizara ya Afya na TAMISEMI, na HelpAge International, limeainisha maeneo makuu yanayoleta kero kwa wazee.
Kwa mujibu wa andiko hilo, changamoto ya kwanza inahusiana na huduma bora ya afya kwa wazee ikiwemo upatikanaji wa dawa. Licha ya Serikali kutoa maelekezo kuwa huduma kwa wazee zitolewe bila malipo na wazee wapewe vitambulisho, changamoto inayojitokeza ni kwamba vitambulisho hivyo vinamwezesha mzee kuhudumiwa katika mkoa kitambulisho kilipotolewa na akiugua akiwa mkoa mwingine, hawezi kupata huduma. Kadhalika dawa za magonjwa yanayowahusu wazee wengi, hasa yale yasiyo ya kuambukiza hazipatikani mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma
``Tunaomba vitolewe vitambulisho vya matibabu kwa wazee vinavyowaruhusu kupata matibabu katika ngazi na vituo vyote na pia tunashauri bodi na kamati za afya katika vituo vya kutolea huduma ziwe na uwakilishi wa wazee ili wafuatilie ununuzi na matumizi ya dawa za wazee,’’ inasema sehemu ya andiko hilo lililoandalikwa na wazee
Kadhalika wazee wanasema sera ya wazee kutotungiwa sheria, kunasababisha mambo mengi kukosa msukumo wa kisheria na hivyo huduma kwa wazee kutolewa kwa hisani na huruma ya kiongozi aliyepo.
Aidha andiko hilo linaainisha msamaha wa kodi ya majengo yanayomilikiwa na wazee kama eneo lingine linaloleta changamoto. Serikali ilitoa msamaha wa kodi ya majengo kwa nyumba zinazomilikiwa na wazee lakini ni kwenye nyumba za kuishi tu na si za biashara. Kadhalika kila mwaka mzee anatakiwa kuandika barua kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kuomba msamaha wa kodi ya majengo.
``Tunashauri ofisi za TRA kote nchini zielekezwe kuzingatia maelekezo ya msamaha huu, elimu itolewe kuhusu msamaha huo na pia mzee akishatambuliwa asamehewe moja kwa moja bila kutakiwa kuandika barua kila mwaka. Pia tunashauri uangaliwe utaratibu wa kusamehe kodi ya ardhi kwa nyumba zinazomilikiwa na wazee, ‘’linasema andiko hilo.
Changamoto nyingine inahusu kipato duni miongoni mwa wazee, kero ambayo wanaishauri Serikali kuangalia namna ambayo wazee wote wenye umri wa zaidi ya miaka 65 watapatiwa pensheni jamii kama inavyofanyika huko Tanzania Visiwani ambako wazee wanapatiwa pensheni.
Eneo lingine ni suala la uwakilishi wa wazee katika vyombo vya maamuzi ambako katika andiko hilo inashauriwa utolewe mwongozo kwa Halmashauri zote kuwaruhusu wawakilishi wa wazee katika vikao vya WDC na Halmashauri nchi nzima ili wazee nao wapate haki yakupiga kura katika vikao hivyo. Kadhalika wanashauri wapate uwakilishi wa mzee katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ili aweze kuwasilisha hoja na kero zao na kufanya masuala yanayohusu kundi hilo yasisahaulike katika mipango na program za maendeleo ya nchi kwa ujuma
Pia katika andiko hilo wazee wanashauri Wizara ya Afya kusimamia utaratibu ili Azimio la Afrika kuhusu haki za Wazee lililokubaliwa tangu Januari 31, 2016 na viongozi wa nchi wanachama ikiwemo Tanzania, litiwe sahihi na hatua zote zinazotakiwa katika kurilidhia.
Kwa mujibu wa andiko hilo, kuridhiwa kwa azimio hilo kutaiweka nchi katika ramani nzuri ya Afrika na dunia kama mojawapo ya nchi zinazotoa kipaumbele na kujali maslahi ya wazee wake.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya wazee nchini ni 2,507,568 (1,200,210 ni wanaume na 1,307,358 wanawake na idadi hiyo ni sawa na asilikia 5.6% ya Watanzania wote ambao kwa mwaka huo ilikuwa 44.9
Dhamira ya Serikali yaleta matarajio makubwa
HelpAge International wana matarajio makubwa kwamba changomoto zinazowakabili wazee zikiwemo hizo zilizoainishwa, zitatafutiwa ufumbuzi wa kudumu na imani hiyo inatokana na hatua kadhaa ambazo zimekuwa zikichukuwa na viongozi mbalimbali wa Serikali kushughulikia masuala ya wazee.
Miongoni mwa mambo yanayoonyesha dhamira ya Serikali kutoa kipaumbele kwa changamoto zinazowakili wazee nchini ni kitendo cha Rais wa awamu ya sita wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuzungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya wazee wa nchi nzima mara baada ya kuingia madarakani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Mei 7 mwaka huu, Rais aliwahakikishia wazee wote nchini kwamba masuala yote yanayowahusu yatashughulikiwa kwa nguvu zote.
Rais Samia alikaririwa akisema kuwa mambo ambayo ni ya kisera watatumia nafasi ya maboresho ya sera yanaayoendelea kufanywa kwa sasa ili sera zinazohusu wazee ziweze kuboreshwa na kuwa na tija.
"Suala lingine ambalo mmelizungumza ni kuhusu afya ya wazee, na hili la afya kwa wazee limezungumzwa vizuri kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo kwa vyovyote vile sina jinsi ya kulikimbia, tutashughulikia masuala yote ya afya ya wazee,’’ Rais Samia alikaririwa akisema.
"Na hapa natoa maagizo kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akasimamie haya leo na si kesho. Tunatambua dunia iko kwenye janga la korona na wanaoathirika zaidi ni wazee, hivyo nataka nitoe taarifa kwa wazee, kamati ambayo nimeiunda itatoa taarifa, ‘’ alisema Rais.