0
Your Cart
No products in the cart.

Kupuuza tahadhari sumu mapambano dhidi ya corona

MLIPUKO wa ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) bado ni tishio duniani na umeathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Athari zake si kiuchumi na kijamii tu bali umegharimu maisha ya watu kwa vifo milioni nne duniani kote. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Na kwa mujibu wa WHO, virusi vya corona vimekuwa vikijibadilisha katika sura tofauti na kusababisha madhara zaidi kwa nchi mbalimbali duniani. WHO licha ya kuendelea kuhimiza watu kuchukua tahadhari kutokana na mabadiliko hayo pia imelenga kufikisha chanjo kwa asilimia 10 ya watu Afrika ifikapo mwishoni mwa Septemba mwaka huu. Inaamini usawa wa chanjo utapunguza tishio la ugonjwa huo. Tayari chanjo milioni 13 zimefikishwa Afrika kutoka kwa mataifa yaliyoendelea lakini idadi hiyo ni ndogo ikizingatiwa Afrika ina watu zaidi ya bilioni 1.3. Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC), kimesema mpaka sasa asilimia 2.4 ndio waliopata chanjo.Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na mlipuko wa wimbi la tatu la virusi vya corona yaani Delta. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za Julai 8, mwaka huu watu 408 walikuwa wamepata maambukizi ya wimbi jipya la Delta huku watu 284 wakipumulia mashine za oksijeni. Wizara imeendelea kusisitiza watu kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kwa kutoa mwongozo ikiwataa wanawe mikono kwa maji tiririka na kujitakasa mikono. Miongozo mingine ni kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima sehemu mbalimbali ikiwemo kupunguza idadi ya abiria katika vyombo vya usafiri (level seat).   Kuvaa barakoa sehemu za mikusanyiko kama sokoni, hospitalini, taasisi za kiserikali na binafsi, vyombo vya usafiri na mikusanyiko mingine. Lakini licha ya kuwepo mwongozo huo watu wamekuwa wakipuuza kuchukua tahadhari hizo za kiafya. TAHADHARI KATIKA VYOMBO VYA USAFIRI Uchunguzi uliofanyika kwa msaada wa Taasisi ya Chimbua umebaini kuwa licha ya watu kuendelea kupata chanjo ya Covid-19, lakini bado wengi wao wanapuuzia tahadhari za kiafya hasa mkoani Dar es Salaam. Mwandishi ameshuhudia idadi kubwa ya watu katika vyombo vya usafiri vya umma na binafsi huku wakiwa hawajavaa barakoa. Hii inaleta taswira kuwa wananchi hawajali namna ya kulinda afya zao dhidi ya mlipuko huo wa Delta. Katika makala haya, mwandishi amezungumza na watu mbalimbali kujua kwanini wanapuuza tahadhari? Husna Faraji ni miongoni mwa wasafiri wanaotumia usafiri wa daladala mara kwa mara kutoka Mbagala hadi kituo cha mabasi cha Mawasiliano Simu 2000. Anashuka kwenye daladala katika kituo hicho huku gari hilo likiwa limejaa bila abiria yeyote kuchukua tahadhari za kiafya za kuvaa barakoa. Analiambia gazeti hili kuwa anaelewa kuwa maambukizi yapo lakini anashindwa kuchukua tahadhari kutokana na kuwahi kazini.   "Kuhusu maambukizi hilo nalijua, nimesikia viongozi wetu wakisema kupitia vyombo vya habari hivyo taarifa ninazo.   "Unajua tatizo linakuja kuwa kuna changamoto ya usafiri nikisema nisubirie basi ambalo halijajaa nitakesha kituoni na kazini nitachelewa kufika hivyo hamna namna nyingine ni kupambana tu,” anasema Faraji anayeuza nguo katika Soko la Mawasiliano.   Abiria mwingine aliyeshuka kwenye daladala linalofanya safari zake kati ya Tegeta Nyuki na Mawasiliano Simu 2000, Shabani Sembaya, anasema anashindwa kuchukua tahadhari kutokana na vyombo vya usafiri kuwa vichache.   "Ninajua kama kuna ugonjwa huo lakini sio mkali. Halafu unajua sisi hatupatwi hovyo na hayo magonjwa kwasababu tangu umeanza sijawahi kupata hata mafua hivyo lazima tuendelee na maisha yetu kama kawaida na tuchukue tahadhari tunapoweza. Tukiufikiria sana tutakwama kimaisha hivyo ni bora tupige kazi,” anasema Sembaya.   Wingi wa abiria katika vyombo vya usafiri haupo katika daladala pekee bali pia katika vyombo vya usafiri vya umma kama mabasi ya mwendokasi lakini huko kila abiria ni lazima anawe mikono kwa maji tiririka au ajitakase na avae barakoa kabla ya kuingia katika basi.   Mmoja wa wasafiri, Eliya Staslaus, anasema: "Kikubwa hapa ni uelewa mdogo na imani ya watu kwasababu hata wakilazimishwa wakiingia ndani wanavua ilihali wamebanana.”   HALI ILIVYO KATIKA MASOKO   Katika soko jipya la kisasa la Kisutu, mwandishi wa makala haya alibaini watu wengi wanaendelea na shughuli zao bila kuchukua tahadhari za kiafya.   Watu wengi walionekana kuingia na kutoka katika soko hilo jipya huku wachache wakiwa wamevaa barakoa. Katika soko hilo hakukuwa na miundombinu ya kunawa mikono kwa maji tiririka.   Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, Anita Sabinius, anasema kutokana na soko hilo kuwa jipya bado hawajawekewa vifaa vya kunawa.   "Soko hili ni zuri na la kisasa lakini bado hatua za kujikinga hazifuatwi watu wanaingia bila kuvaa barakoa na hata mikono hawanawi. Naelewa kama ugonjwa upo na serikali ilishasema tujikinge lakini hilo limepuuzwa," anabainisha Anita.   Katika Soko la Ilala hali haitofautiani na soko la Kisutu, huko pamoja na kuwepo miundombinu ya kunawa mikono, watu wachache walionekana kuitumia.   Katika Soko Kuu la Samaki Feri idadi ya watu waliingia na kutoka huku ulazima wa kunawa mikono ukiwepo lakini licha ya kuchukua tahadhari hiyo kundi la wanawake walioingia kununua samaki walionekana katika mikusanyiko wakizunguka meza bila tahadhari yoyote.   Mmoja wa wanawake hao, Mwanaisha Abdul, anasema anaamini kuwa ugonjwa huo haupo tena na maisha lazima yaendelee huku akisisitiza watu wazidi kumuomba Mungu kwa bidii. MUTAFUNGWA: CHANGAMOTO NI HII Miongoni mwa chombo muhimu katika kudhibiti idadi ya watu katika vyombo vya usafiri ni Kikosi cha Usalama Barabarani. Kamanda wa kikosi hicho nchini, Wilbroad Mutafungwa, anasema kisheria idadi ya watu inapaswa kudhibitiwa. “Kwenye magari sisi tunachukua hatua na ndio maana magari ya mikoani hayajazi watu na kuhusu mijini tumeweka askari vituo vya daladala kuhakikisha madereva, makondakta na abiria wanavaa barakoa. Akijibu swali kwanini pamoja na kuwepo sheria watu bado wanajaa kwenye vyombo vya usafiri bila kuchukua tahadhari, Mutafungwa anasema: “Changamoto zinakuja nyakati za asubuhi na jioni watu wanakuwa wengi wanaohitaji usafiri lakini magari yanayotoa huduma hayatoshi hivyo tutakapochukua hatua watu wengi watabaki vituoni. Anasema suluhu kubwa kwao ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ikibidi wachukue vyombo vya usafiri vya mbadala ili kujikinga na kuhakikisha wanavaa barakoa. WANACHOKIFANYA LATRA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Giliard N’gewe, anasema mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachukue tahadhari za kiafya wanapotaka kupanda katika vyombo vya usafiri. “Sisi tuna jukumu la kuwaelimisha abiria na tunafanya hivyo nchi nzima kwa kila kituo hata ukienda Mbezi Louis utakuta tunatoa elimu. “Pia tunawaambia wafanyakazi wa vyombo vya usafiri wasiruhusu mtu kuingia  ndani ya basi bila kuchukua tahadhari  za kiafya, kuhusu mwendokasi tumewaambia Dart wasimamie idadi ya watu wasizidi hivyo kikubwa tunachokifanya ni kutoa elimu,” anafafanua N’gewe. DART MABASI 70 YATASAIDIA Meneja Uhusiano wa Wakala wa magari yaendayo haraka Dar es Salaam (DART), William Gatambi, anasema kwa kawaida magari hayo yanaruhusiwa kubeba abiria 140 hadi 160 kwa basi la mita 18 ambalo lina viti 40. “Kwa muundo wa basi hivyo viti vilivyoko ni vya watu wasiokuwa na uwezo wa kusimama kama wazee, walemavu, wajawazito na wanaonyonyesha wengine wote wanatakiwa kusimama kutokana na usafiri huo kutumia muda mfupi na masafa mafupi,” anasema Gatambi aliyesisitiza uvaaji barakoa katika usafiri huo ni wa lazima. Anasema magari yaliyoletwa hivi karibuni yatasaidia kupunguza misongamano katika mabasi hayo. “Yameshaingia barabarani na yanaendelea na safari hivyo yatasaidia kupunguza misongamano lakini tahadhari zingine zinatakiwa kufuatwa,” anaeleza. KINACHOFANYIKA MASOKONI Ofisa Masoko wa Jiji la Dar es Salaam, Victor Rugemalila, anasema wanachofanya ni kutoa elimu ya tahadhari kutokana na watu wengine kupuuzia na kuingia sokoni bila kunawa na kuvaa barakoa licha ya kuwepo na miundombinu ya kunawa mikono. “Katika awamu iliyopita tuliweka vitakasa mikono na maji ya kunawa yenye dawa na hivi vipo katika masoko yote isipokuwa soko jipya la Kisutu bado hatujaweka kwasababu soko bado jipya na harakati za kuhamisha wafanyabiashara wa Kariakoo. Anasema watu wanaoingia sokoni wanapewa elimu ikiwemo kuvaa barakoa ila changamoto ni imani waliyojiwekea. “Wito wangu ni kwamba pamoja na kuwa na imani wajikinge katika maeneo hayo,” anasema Rugemalila. JE, CHANJO ITAFANIKIWA? Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mapafu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Elisha Osati, anasema ni muhimu kuchukua tahadhari hata baada ya kupata chanjo kutokana na maambukizi kuwa na uwezo wa kusambaa. “Faida kubwa ya chanjo ni kumfanya mtu asipate ugonjwa mkali ambao unaweza kuleta uharibifu katika mapafu hivyo ni muhimu watu kuzingatia tahadhari kama kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko hata kama wamechanja la sivyo ugonjwa utaendelea kusambaa,” anabainisha. MPANGO WA WIZARA Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi, anasema licha ya kutoa mwongozo wa kujikinga serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi sehemu zote kuhakikisha wanachukua tahadhari bila kuathiri shughuli za maendeleo na umuhimu wa kupata chanjo. “Nasisitiza pamoja na kupata chanjo watu wasisahau kuchukua tahadhari za kiafya kwani ni muhimu kujikinga wasipate virusi,” anasisitiza Profesa Makubi. Hapa nchini dozi zaidi ya milioni moja zilipokewa nchini na mpaka kufikia Agosti 28, mwaka huu watu 304,603 wamepata chanjo, kati yao wanaume ni asilimia 66 na wanawake ni asilimia 33. Utoaji chanjo ulizinduliwa mwishoni mwa Julai, mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan.

Add a Comment

Your email address will not be published.

All Categories

Get Free Consultations

SPECIAL ADVISORS
Quis autem vel eum iure repreh ende